POLE sana! Tatizo la kutoshika mimba (infertility) au kushindwa kupata mimba (conceive) limekuwa likimtesa staa wa Bongo Movies, Beautiful Onyinye, Wema Isaac Sepetu na limehusishwa na ugumba.
Akizungumza na Amani juu ya ishu hiyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Wema alisema suala la kutopata mtoto limekuwa likimkosesha amani katika maisha yake ya ukubwani.
ASHINDA AKILIA
Alisema kwamba, amekuwa akishinda akilia kila anapokutana na shosti wake wa sasa, Aunt Ezekiel ambaye ni mjamzito.Wema alitiririka kwamba, kila wakati amekuwa akimwambia Aunt kuwa na yeye anatamani kupata mimba lakini Mungu hajamjalia. Kwa kusema hivyo, huwa wanajikuta wakikumbatiana na kuangua vilio wote kwa pamoja.
TATIZO UMRI UMEENDA
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa mkali huyo wa sinema za Kibongo ambaye pia ni Miss Tanzania 2006, mwanadada huyo anaona umri umeenda sana kwani tayari ana miaka 26 sasa.
"Unajua Wema alishajaribu kupata mtoto mara kadhaa ikashindikana na umri nao unakwenda hivyo lazima akose amani. Hebu fikiria aliwahi kuwa na Kanumba (marehemu Steven), Jumbe (Yusuf), Chaz Baba (Charles Mbwana) na Diamond (Nasibu Abdul) lakini kote huko alitoka kapa.
YAMKUTA YA JIDE
"Mbaya zaidi ni maneno yanayosemwa na watu yanamuumiza sana, wanasema ni mgumba kama ilivyokuwa kwa Jide (mwanamuziki Judith Wambura 'Jaydee')."Kwa kweli hali hiyo inamtesa sana ila watu hawajui bora wakafunga vinywa vyao na kuacha kuandika kwenye mitandao ya kijamii," alifunguka mtu huyo wa karibu.
AKIWAONA MA-MISS TZ WENZAKE WANA WATOTO KILIO
Chanzo hicho kiliendelea kufunguka kwamba, Wema amekuwa akilia kila anapowaona ma-Miss Tanzania wenzake wakiwa na watoto wao.
Ilisemekana kwamba warembo ambao wanamliza ni Wema Nancy Sumary (Miss Tanzania 2005), Faraja Kota (2004), Hoyce Temu (1999), Jacqueline Ntuyabaliwe 'K-lynn' (2000) na Miriam Gerald (2009).
Ilisemekana kwamba wengine aliokuwa nao kwenye shindano hilo mwaka 2006 ambao wana watoto ni Lisa Jensen, Aunt Ezekiel na wengine ambao kwa pamoja wamekuwa wakimfanya naye atamani kupata mtoto.
DAKTARI AELEZA
TATIZO KWA KINA
Akielezea tatizo hilo kwa kina, Dk. Fadhili Emily wa Kitengo cha Tiba ya Sayansi cha The Fadhaget Sanitarium Clinic kilichopo Mbezi-Africana jijini Dar alisema:"Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, wanandoa asilimia 50 wanapata mimba ikiwa watajamiiana bila kutumia kinga, wakifanya tendo hilo ndani ya miezi mitatu, asilimia 75 baada ya miezi sita na asilimia 95 baada ya mwaka mmoja lazima kuwe na matokeo kama hakuna kuna tatizo.
NINI SABABU?
"Sababu za tatizo la kutopata mimba ni nyingi sana na baadhi yake ni hizi zifuatazo:
"Matatizo ya mbegu za kiume (sperm disorders).
"Asilimia 35 ya wanaume wana tatizo hili na lingine ni kutopevuka kwa mayai kwa wanawake kitaalam huitwa ovalatory dysfunction.
"Matatizo mengine ni yale yasiyo ya kawaida ya ute wa shingo ya uzazi ambapo ni asilimia 5 tu.
"Wengine huwa na matatizo ya homoni na wapo wanawake ambao hawapati mimba na sababu zao hazijulikani, hawa ni asilimia 10."
MSONGO NA
WASIWASI
"Wengine ni kutokana na kuwa na msongo na wasiwasi. Tatizo lingine la mwanamke kutoshika mimba husababishwa na hitilafu katika mirija ya uzazi (tubal dysfunction), hawa huwa asilimia 30. Wanawake wenye tatizo hili wanashauriwa kuhudhuria kliniki za akina mama ili waonane na madaktari.
"Lakini pia wanashauriwa kufuatilia siku zao za mzunguko wa hedhi na tendo la ndoa mara kwa mara hasa baada ya siku 10 kutoka siku anapomaliza hedhi na aanzie siku ya kwanza ya kupata hedhi.
"Pia wanawake wanashauriwa wawe wanapima joto la mwili asubuhi na jioni kipindi cha kushika mimba na kama litaongezeka kwa nyuzi joto 0.5 wanashauriwa kipindi hicho kufanya tendo la ndoa."
KWA ULAYA NA MAREKANI
"Kwa nchi za Ulaya na Marekani wana kipimo cha kuonesha siku ambayo yai litapevuka, hivyo mtu kuwa na uhakika na siku ya kupata mimba akiamua. Kipimo hicho kinaitwa luteinizing hormone prediction test kits.
"Pia wanawake wanaotaka kupata mimba wanashauriwa kuepuka ulevi na uvutaji wa sigara kupindukia. Lakini hata wale wenye mimba wanashauriwa kuepuka vitu hivyo."
UGUMBA NA UTASA
Dokta huyo aliendelea mbele na kusema ugumba ni tatizo linaloweza kuondoka kwa mtu siku moja. Na mgumba ni mwanamke au mwanaume na ni yule mtu ambaye umri wake wa kuzaa umefikia lakini hawezi kutunga mimba (kwa mwanaume) au kutungwa mimba (kwa mwanamke).Alisema tasa ni viumbe wote, hata wanyama wanaweza kuwa tasa lakini wanyama hawawezi kuwa wagumba.